Hayo yameelezwa  leo jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt Alphonce Chandika, wakati akitoa salamu za Hospitali kwa washiriki wa matembezi ya hisani mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Saimon Odunga ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge katika maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani ambayo kimkoa yamefanyika leo 29 Septemba, 2018 katika viwanja vya Hospitali ya Benjamin Mkapa.

“Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyoambukiza kama yalivyo magonjwa ya moyo, kila mwaka huuwa watu milioni 38 duniani. Vifo vingi kati ya hivyo, hutokana na magonjwa ya moyo”. Asema.

Inakadiriwa kwamba watu takriban milioni 17.5 hufariki dunia kila mwaka kwa magonjwa hayo ya moyo, ikifuatiwa na magonjwa ya Saratani yanayouwa watu takriban milioni 8.2 kwa mwaka, wakati magonjwa ya njia ya hewa yanauwa watu milioni nne na Kisukari watu milioni 1.5 kila mwaka, amesisitiza Dkt. Chandika.

“Magonjwa hayo huenda sambamba na saratani ambayo huuwa watu milioni 8.2 kwa mwaka huku magonjwa ya njia ya hewa yakichangia vifo vya watu milioni 4 na ugonjwa wa kisukari ukisababisha vifo vya watu takribani milioni 1.5 kila mwaka”.

Kwa upande wa Tanzania, takwimu kutoka Chama cha Madaktari wa Watoto nchini (PAT), zinaonyesha kwamba takriban watoto 13, 600 huzaliwa kila mwaka wakiwa na magonjwa aina mbalimbali ya moyo, huku watoto takriban 3, 400 kati yao, wakihitaji kupatiwa matibabu kwa kufanyiwa upasuaji.

“Watoto 13,600 nchini, wanazaliwa wakiwa na magonjwa ya Moyo na kati yao, 3,400 wanahitaji matibabu ya upasuaji”. Amebainisha.

Sambamba na hayo, Mkurugenzi huyo Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin MKapa alinukuu Takwimu za Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto zilizotolewa na Waziri wa Wizara hiyo Mh. Ummy Mwalimu katika Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa (Third UN High level Meeting) uliofanyika hivi karibuni kwamba asilimia 34 ya vifo nchini Tanzania kila mwaka husababishwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambapo Moyo ni moja wapo.

Mbali na hayo Dkt Chandika amebainisha sababu zinazosababisha magonjwa ya moyo. “Watu wengi hupatwa na magonjwa ya moyo kwasababu hawazingatii kanuni za ulaji wa vyakula bora ikiwemo ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, chumvi nyingi, sukari nyingi, uvutaji wa sugara, unywaji pombe kupita kiasi pamoja na kutokufanya mazoezi mara kwa mara”.

Kwa upande wake  Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Saimon Odunga, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, ametoa wito kwa Watanzania kujenga tabia ya kupima afya zao na kula mlo kamili.

“Watanzania wengi wamekuwa wakishindwa kupima afya zao huku wakitumia vyakula hatarishi wakiamini kuwa kutumia vyakula vyenye mafuta mengi na kuwa mnene ni dalili ya uwezo wa kiuchumi kumbe ni kujiweka Katika mazingira hatarishi,” amesema.

Mkuu huyo wa wilaya alitoa historia ya magonjwa hayo kwamba zamani iliaminika kuwa magonywa ya moyo ni magonywa ya kitajiri jambo ambalo si kweli kwani takwimu zinajionesha wazi kuwa magonjwa hayo humpata yeyote kwani yanatokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha hususan kutozingatia ulaji bora na kutofanya mazoezi.

“Kuwa na afya bora si unene. Ni matokeo ya kutozingatia ulaji mzuri. Kula mlo kamili hakuitaji kuwa na kipato kikubwa bali hata Mtanzania mwenye kipato kidogo ana uwezo wa kula mlo kamili,” amesisitiza.

Hospitali ya Benjamin ilipewa jukumu la kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya siku ya Moyo duniani kwa jiji la Dodoma yaliyofanyika leo tarehe 29.09.2018 katika viwanja vya hospitali. Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo “MOYO WANGU, MOYO WAKO” yalitanguliwa na matembezi ya hisani na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Saimon Odunga, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge.

Baadhi ya wagonjwa wakisubiri kupima magonjwa ya moyo

Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Chemba Saimon Odunga akichukuliwa damu na muuguzi Mecktilda Mashauri kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo.

Wafanyakazi wa hospitali ya Benjamin Mkapa wakifanya maandamano kuadhimisha  Siku ya Moyo.

Imeandaliwa na
Kitengo cha Uhusiano na Masoko.

CategoryNews

Copyright © 2018 - Benjamin Mkapa Hospital All rights reserved

Privacy Policy    |   Disclaimer   |    Sitemap