Kutoka kwa Mkurugenzi
Published on August 11, 2022
Karibu kwenye Tovuti ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH)
Tangu kuanzishwa kwake na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 13 Oktoba 2015, Hospitali ya Benjamin Mkapa imekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma za kisasa za afya. BMH ni taasisi ya umma ya ngazi ya juu (tertiary), ya rufaa na mafunzo ya chuo kikuu, iliyoanzishwa kwa lengo la kutoa huduma za afya za juu na maalum kwa Watanzania na Afrika kwa ujumla kupitia ununuzi wa vifaa vya kisasa vya uchunguzi, wataalamu wenye ujuzi na matibabu ya hali ya juu.
Hospitali hii ipo Dodoma, ambayo ni makao makuu ya nchi, na ndiyo Hospitali Kuu ya Serikali katika jiji hilo, ikihudumia takribani watu milioni 14. BMH iko chini ya Wizara ya Afya na inafanya kazi kwa karibu na Chuo Kikuu cha Dodoma. Pia, BMH ina ushirikiano mpana na taasisi nyingine ndani ya Afrika, Ulaya, Mashariki ya Kati, Asia na Amerika.
Tunatoa huduma bora za afya za kibingwa na ubingwa wa juu, ambazo hapo awali hazikuwepo nchini, kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kitabibu. BMH inamiliki vifaa vya kisasa kabisa kama vile mashine ya CT Scan (Computed Tomography), MRI (Magnetic Resonance Imaging), na Maabara maalum ya Moyo (Cardiac Catheterization Laboratory).
Mbali na huduma za kibingwa, tunatoa matibabu ya kina kwa magonjwa ya figo pamoja na Upandikizaji wa Figo, upandikizaji wa Uloto wa mfupa na huduma za Hematolojia, upandikizaji wa Uume, matibabu ya moyo na upasuaji wa Moyo wazi, Upasuaji wa Ubongo, Mifupa na Majeraha, Saratani, Mionzi ya Saratani, Tiba ya Nyuklia, pamoja na upasuaji wa matundu madogo (Laparoscopy) na Endoscopy.
Zaidi ya huduma za kitabibu, BMH inatoa mafunzo ya udaktari wa chuo kikuu, inafanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu. Pia, hospitali inatoa huduma za utalii wa kimatibabu kwa wagonjwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika.