Mwanzo / Huduma Zetu / BALOZI WA NORWAY ARIDHISHWA NA HUDUMA BMH

BALOZI WA NORWAY ARIDHISHWA NA HUDUMA BMH

Published on March 01, 2023

Article cover image

Balozi wa Norway nchini, Bi Elisabeth Jacobsen, ameridhishwa na huduma za afya katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma.

Akiwa katika ziara ya kutembelea miradi inayotekelezwa Dodoma ili kujiridhisha na tamko la serikali kwa mabalozi kuhamia makao makuu ya nchi, Bi Elisabeth alifika katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Kanda ya Kati Februari 27 majira ya mchana akiambatana na ujumbe wake wenye watu 23 kutoka ubalozini.  

"Huduma zenu ni nzuri, chumba hiki ni kinavutia, madhari ya hospitali yanavutia, na tumeona vifaa vya kisasa" alisema Bi. Elizabeth alipooneshwa baadhi ya vyumba wanavyotumia viongozi wanapokuwa wamelezwa Hospitalini hapo.                                                                                                

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mheshimiwa Jabir Shekimweli alimhakikisha balozi huyo kuwa, Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, umefanyika uwekezaji mkubwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, ikiweo kuongeza huduma na vifaa tiba vya kisasa kuiwezesha kuwahudumia viongozi wa ngazi zote wakiwemo Waheshimiwa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini.

“Kuna vifaa kama MRI na CT-Scan matoleo ya kisasa, kuna mradi wa kituo cha mionzi tiba, na huduma nyinginezo kama utakavyo jionea baadaye” Alisema Mheshimiwa Shekimweli.                                            

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt. Alphonce Chandika alitoa taarifa fupi kuhusu huduma zinazotolewa na Hospitali hiyo kwamba ni Pamoja na huduma zote za kibingwa na ubingwa bobezi.

“Tunatoa huduma nyingi za ngazi ya Kibingwa na Ubingwa Bobezi, ikiwa ni pamoja na huduma za kupandikiza Figo, Huduma za magonjwa ya Moyo kwa kutumia maabara maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo Cath-lab, na Huduma za Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu” alieleza Dkt. Chandika.

Hospitali ya Benjamin Mkapa inaendelea kupanua huduma zake, ikipanga kujenga kituo cha matibabu ya Moyo, kituo cha Upasuaji wa Ubongo,Uti wa mgongo na Mifupa, Kituo cha Mama na Mtoto, na Kituo cha Magonjwa ya Dharula, Pamoja na kituo cha tiba za Upandikizaji  wa Viungo miongoni mwa mipango ya baadaye.