HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA (BMH) YA KWANZA KATIKA SEKTA YA UMMA KUFANYA UPASUAJI WA JICHO KWANJIA YA MATUNDU MADOGO
Published on March 13, 2025

Na. Jeremiah Mbwambo, Dodoma, 13/03/2025
Hospitali ya Benjamin Mkapa imekuwa Hospitali ya kwanza katika sekta ya Umma kwa kufanya upasuaji (Operation) kwa njia ya matundu madogo.
Mkuu wa Idara Dkt. Jacinta Feksi amesema mpaka kufikia leo wameona wagonjwa 1020 katika magonjwa mbalimbali ya macho.
"Jambo ambalo tunajivunia ni kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo ya macho kwa njia ya upasua(Operation) wa matundu madogo ili kuondoa mtoto wa jicho" amesema Dkt. Jacinta
Ameongeza kuwa njia hii inafaida kubwa kwa mgonjwa kiuchumi na kiafya
"Hospitali ya Benjamin Mkapa itatoa matibabu haya kwa gharama ndogo ukilinganisha na maeneo mengine, hata hivyo njia hii humsaidia mgonjwa kupona marabaada ya upasuaji kufanyika na mgonjwa huruhusiwa siku hiyo hiyo" amesema Dkt. Jacinta
Kwa upandewake Daktari Bingwa wa magonjwa ya macho na mhadhiri wa chuo Kikuu cha Dodoma Frank Sandi ameeleza ushirikiano wa madaktari Bingwa wa macho kutoka marekani (Morani) ni wa muda mrefu unazaidi ya miaka tisa sasa.
"Ushirikiano wa chuo cha UDOM, BMH na Morani unaleta matokeo chanya ya kuwa hudumia watanzania kwa teknolojia ya hali ya juu, lakini pia inatujengea uwezo kwa madaktari na Wataalamu wengine" Amesema Dkt. Frank
Aidha kiongozi wa Msafara wa Madaktari Bingwa wa Macho Morani Dkt. Jeff Pettey amesema ni fahari kuwepo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa na kuona jinsi wataalamu wanavyo endelea kuwahudumia wananchi.
"Tumekuja hapa mara kadhaa na kuona uwekezaji mkubwa uliofanyika lakini pia wataalamu walivyo na moyo wakutoa huduma hii inatupa nguvu ya kuendelea kuwa karibu na wataalamu wa Hospitali na Chuo Kikuu cha Dodoma" Amesema Dkt. Jeff.