HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA (BMH) NA TAASISI YA MORAN EYE CENTER YA MAREKANI WAKUBALIANA KUKUZA ZAIDI USHIRIKIANO ILI KUIJENGEA UWEZO IDARA YA MACHO YA BMH
Published on March 12, 2025

Na Jeremia Mwakyoma.
DODOMA - Machi 5, 2025
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na taasisi ya Moran Eye Center ya Chuo Kikuu cha Afya cha Utah cha nchini Marekani wamekubaliana kuendeleza zaidi ushirikiano na kuendelea kuijengea uwezo zaidi idara ya matibabu ya macho ya BMH.
Hayo yamebainishwa leo wakati Mkurugenzi wa Hospitali ya BMH Prof Abel Makubi alipokutana na kuzungumza na Ujumbe wa Taasisi hiyo ya Moran Eye ambao wamekuja BMH na kwa kushirikiana na Madaktari Bingwa wa Macho wa BMH kwa pamoja wameweka kambi ya Uchunguzi wa magonjwa ya macho kwa wananchi inayofanyika kuanzia Machi 5 hadi 7, 2025 na kisha kufanya upasuaji wa macho kuanzia Machi 10 hadi 14, 2025.
Akitoa salamu za kuushukuru ujumbe huo kutoka Marekani, Prof. Makubi amebainisha kuwa ushirikiano uliopo kati ya BMH na Moran Eye Center utasaidia wataalamu wa pande zote mbili kujifunza kutoka kwa kila mmoja na kujengeana uwezo katika utaalamu wa matibabu ya macho, masuala ya utafiti, huduma za Afya Mkoba kwa jamii (outreach programme) hususani kwenye maeneo ambayo ni vigumu wananchi kuweza kufika kwenye vituo vya Afya na Hospitali kubwa.
"Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa msaada wa mashine na vifaa tiba ambavyo taasisi ya Moran Eye Center ilichangia katika idara ya matibabu ya macho ya BMH na ushirikiano ambao umeendelea kuwepo kati ya Taasisi zetu hizi mbili, utasaidia wataalamu wetu kuweza kujengeana uwezo na kubadilishana uzoefu katika maeneo ya matibabu ya macho, mafunzo kwa wataalamu, masuala ya utafiti na huduma za Afya Mkoba kwenye jamii" alisisitiza Prof. Makubi
Prof Makubi aliitaja Dodoma kama moja ya Mikoa yenye kiwango kikubwa cha matatizo ya macho na kuongeza kuwa mpango wa Serikali ni kuifanya BMH kuwa na Idara ya macho yenye uwezo wa ubingwa wa juu kuweza kukabiliana na tatizo hilo ili wananchi wanaokuja kutibiwa macho wapate huduma za ubingwa wa juu wa matibabu ya macho.
"Tunataka asilimia 99 ya Wagonjwa wanaokuja BMH kupata matibabu ya macho, wote wawe wanatibiwa na kumaliza changamoto zao za macho hapa hapa BMH bila kuhitaji kwenda Hospitali zingine" alisisitiza Prof. Makubi.
Ni matarajio yangu kuwa ushirikiano uliopo kati ya BMH na Taasisi ya Moran Eye Center utaendelea kukua zaidi kwa kuzingatia BMH inaendelea kukua na kwa kutambua kuwa Serikali imehamia Dodoma kutoka Dar es salaam hivyo matarajio ya Serikali na Wananchi ni Makubwa juu ya huduma za Afya zinazotolewa na BMH.
Nae Mkuu wa Idara ya Macho na Daktari Bingwa wa Macho wa BMH Jacinta Feksi amesema kuwa ushirikiano kati ya BMH na Moran Eye Center ulianza tangu mwaka 2016 na kuwa pamoja na maeneo mengine ambayo taasisi hiyo imefadhili, wanatarajia itasaidia katika kufadhili mradi wa ujenzi wa Jengo la matibabu ya macho na katika kuanzisha banki ya Kioo cha Jicho (Cornea Bank) ili kuifanya BMH kuwa hospitali ya kwanza nchini kuwa na Benki hiyo na kuwezakushughulikia matatizo ya vioo vya macho kwa wananchi.
Kwa upande wake Bi Lori Mccoy ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Mkoba katika Taasisi ya Moran Eye Center amesema kuwa watasaidia pia katika mafunzo na utafiti juu ya magonjwa kama presha ya macho (Glaucoma) na kuleta Madaktari Bingwa na wako tayari kukuza zaidi ushirikiano na BMH kadiri itakavyoweza kusaidia BMH katika idara ya macho, pia ameshukuru kwa kupata fursa ya kutembea kwenye Maeneo ya Baadhi ya Wilaya za Dodoma kupeleka huduma za Afya Mkoba na ameahidi timu ya Wataalamu zaidi watakuja BMH kwa ajili ya Programu za upasuaji wa macho zitakazoanza tarehe 10 hadi 14 Machi 2025.