Mwanzo / Huduma Zetu / WAZIRI WA AFYA MHE JENISTA MHAGAMA (MB.) APONGEZA HUDUMA ZA AFYA ZA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA KATIKA MAONESHO YA WIKI YA AFYA

WAZIRI WA AFYA MHE JENISTA MHAGAMA (MB.) APONGEZA HUDUMA ZA AFYA ZA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA KATIKA MAONESHO YA WIKI YA AFYA

Published on April 09, 2025

Article cover image

Na Jeremia Mwakyoma
Picha na Gladys Lukindo na Carine Senguji
DODOMA - APRILI 8, 2025 

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama (MB) amepongeza na kuonesha kuridhishwa na huduma za Afya zinazotolewa kwenye Banda la Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) katika Maonesho ya Wiki ya Afya yanayofanyika katika Viwanja vya ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Jijini Dodoma. 

Mhe. Jenista ameyasema hayo leo alipotembelea banda la BMH kujionea hali ya utoaji huduma kwa wananchi wakati wa hafla ya kilele cha Maonesho ya Wiki ya Afya yanayohitimishwa leo Jijini Dodoma. 

"Ni jambo la kuridhisha kuona timu ya Madaktari Bingwa, Wabozezi na mashine za kisasa za kufanyia vipimo na kutolea matibabu ambazo Hospitali ya Benjamin Mkapa imezileta kwenye Maonesho ya Wiki ya Afya kwa ajili ya kuhudumia Wananchi; Aidha, nipongeze pia kwa namna maonesho yalivyoandaliwa na kutangazwa vizuri yameweza hadi kuwaleta Wananchi wa Mikoa mbalimbali kuja kutembelea Maonesho na kupata huduma za matibabu" alisisitiza Mhe. Waziri Jenista. 

Nae Daktari Bingwa na Mkuu wa Idara ya magonjwa ya mfumo wa mkojo wa BMH Dkt. Remigius Rugakingira amemwelezea Waziri Jenista kuwa, pamoja na vipimo vya kisasa, BMH imeleta Madaktari Bingwa katika magonjwa ya Figo, magonjwa ya Moyo, magonjwa ya Damu na huduma za upandikizaji Uloto, Magonjwa ya macho, Magonjwa ya mfumo wa mkojo, magonjwa ya ndani na huduma za afya za dharura. 

"Hadi kufikia jana, tayari BMH ilikuwa imehudumia Wananchi zaidi ya 320 na bado idadi ya Wananchi wameendelea kujitokeza kwa Wingi siku ya leo ambayo ndio kilele" aliongeza Dkt. Remigius


Mama Magreth Kusekwa wa Ipagala Jijini Dodoma ameshukuru kwa huduma za matibabu ya macho  alizozipata kwenye banda la BMH, huduma hazichelewi ndani ya muda mfupi unakuwa umekamilisha matibabu yako. 

Aidha, amepongeza Wizara ya Afya kwa kuandaa maonesho ya Afya na kuzileta Taasisi nyingi za kutoa huduma za Afya chini ya mwamvuli mmoja imekuwa rahisi kwa wananchi, tunaomba maonesho haya yafanyike kila mwaka. 

Nae Imma Mwehanga Mkazi wa Nkuhungu Dodoma ameelezea kuridhishwa kwa juhudi za Serikali kutuwekea huduma za pamoja kwenye eneo hili la Jakaya Kikwete Convention, nimepata fursa ya kupima vipimo vya moyo vya ECHO na ECG, kwakweli Afya ndio mtaji wa kwanza, wananchi wasipuuzie suala la kuja kucheki Afya hadi waugue walale kitandani, Maonesho haya ya huduma za Afya yawe angalau mara mbili kwa mwaka.