Mwanzo / Huduma Zetu / HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA KATIKA UTOAJI WA HUDUMA BORA ZA AFYA MWAKA 2025 KWA NGAZI YA HOSPITALI ZA RUFAA ZA KANDA

HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA KATIKA UTOAJI WA HUDUMA BORA ZA AFYA MWAKA 2025 KWA NGAZI YA HOSPITALI ZA RUFAA ZA KANDA

Published on April 09, 2025

Article cover image

Na Jeremia Mwakyoma
Picha na Carine Senguji na Gladys Lukindo
DODOMA -APRILI 8, 2025


Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) leo imetunukiwa Tuzo ya kuwa Mshindi wa Kwanza katika utoaji wa huduma bora za Afya kwa mwaka 2025 kwa kundi la Hospitali za Rufaa za Kanda zote nchini. 

Tuzo hiyo imetolewa leo na Wizara ya Afya katika hafla za kilele cha Wiki ya Afya Kitaifa mwaka 2025 iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa  Jakaya Kikwete uliopo Jijini Dodoma. 

BMH imetunukiwa Tuzo hiyo baada ya mchakato wa kuzishindanisha Hospitali zote za Kanda hapa nchini na kuibuka Mshindi katika mchakato huo ulioendeshwa na kusimamiwa na Wizara ya Afya na kisha kuzipiku Hospitali zote za Kanda hapa nchini kwa kutoa huduma bora za Afya. 


Akitambulisha Tuzo hizo Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema kuwa katika maadhimisho ya Wiki ya Afya kwa mara ya kwanza Kitaifa limefanyika tukio la kuwatia moyo na kutambua mchango mkubwa wa watoa huduma za Afya kuanzia ngazi za msingi hadi Taifa na kuendesha mchuano kwa kushirikiana kati ya Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI ili kupata Hospitali zilizofanya vizuri.


"Kwa upande wa Hospitali za Rufaa ngazi ya Kanda tumepata mshindi  mmoja ambaye ni Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo jijini Dodoma" alitangaza Dkt. Magembe jambo ambalo liliibua shangwe ukumbi mzima miongoni mwa Wajumbe walioshiriki hafla ya kilele cha Wiki ya Afya. 

Dkt. Magembe anasema katika mchakato wa kuzishindanisha Hospitali waliangalia kiwango cha utoaji huduma za Afya na "Customer Care" na kuona namna Wagonjwa wanavyoridhishwa na huduma, lakini pia vigezo vya huduma za lishe na Ustawi wa jamii, uwajibikaji, usafi wa Mazingira, upatikanaji wa Dawa, Vifaa na Vifaa tiba na kiujumla ubora wa huduma za Afya ambazo zinatolewa na Hospitali na hatimae Hodpitali ya Benjamin Mkapa kuibuka mshindi. 

Akikabidhi tuzo hizo, pamoja na kutoa pongezi Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama alitumia mkutano huo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kusema kuwa amekuwa kama Daktari Bingwa Mbobezi namba moja kwa mabadiliko (Reforms) kubwa alizozifanya katika Sekta ya Afya ikiwemo kuweka Vifaa tiba vya teknolojia ya kisasa ya kibingwa na kibobezi na Madaktari wenye ubingwa na ubobezi wa kutoa tiba na kufanya uchunguzi wa teknolojia za kisasa. 

"Rais pia ameanzisha Scholarship maalum ya masomo ya ngazi za ubobezi ili kuwajengea uwezo madaktari wetu na Watoa huduma za Afya wengine  ili kuleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya Afya hapa nchini na hadi sasa Mhe Rais ameshatumia zaidi ya shilingi Bil. 30 kuwasomesha Madaktari maeneo yote ya kimkakati" alimaliza Mhe. Mhagama. 

Nae Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa leo hususani Sekta ya Afya kupitia kilele cha Wiki ya Afya Kitaifa tunasherehekea mambo makubwa ambayo yamefanywa na Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sekta ya Afya huku akipongeza kazi kubwa inayofanywa na hospitali za Rufaa za Taifa, za Kanda, Mikoa, Wilaya Vituo vya Afya hadi ngazi za chini na Wataalamu wote waliopo katika sekta ya Afya na Wadau wanaounga Mkono maendeleo ya Sekta ya Afya.