Mwanzo / Huduma Zetu / BILLION 2.7 YAENDELEA KUOKOA WATOTO WENYE UGONJWA WA SELIMUNDU TANZANIA

BILLION 2.7 YAENDELEA KUOKOA WATOTO WENYE UGONJWA WA SELIMUNDU TANZANIA

Published on June 20, 2023

Article cover image

Bw. Jeremiah Mbwambo Msemaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ameeleza, kila ifikapo Juni 19 Dunia huadhimisha Siku ya Selimundu.

“Siku hii ni maalum na inaadhimishwa duniani kote na siku hii ilipitishwa mwaka 2008 na mkutano mkuu wa umoja wa mataifa ambapo selimundu ilitambulika kama janga la Dunia, kwa kutambua ukubwa wa tatizo hilo Serikali kupitia wizara ya Afya imekuwa mstari wa mbele kwa kuwekeza kiasi cha shillingi bilioni 2.7 kwaajili ya matibabu ya Watoto wenye selimundu.

"Matibabu ya ugonjwa wa selimundu yameshaanza katika Hospitali ya Benjamin Mkapa na huduma hiyo ilizinduliwa rasmi nchini mnamo Mei 10, 2023 na mpaka sasa Watoto watatu wameshapatiwa matibabu na huku mmoja akiendelea na matibabu hivyo kufanya idadi ya Watoto wanne" alisema Jeremiah.

Dkt. Stella Malangahe ambae ni daktari bingwa wa magonjwa ya damu kutoka BMH ameeleza kuwa siku hii ni maalum kuangalia namna wagonjwa wa selimundu wanavyoendelea na hali zao lakini pia ni nafasi kwa watoa huduma kuangalia namna gani wanaweza kuboresha afya za wagonjwa.

“Ugonjwa wa selimundu ni ugonjwa wa kurithi kutoka kwa wazazi ambapo mgonjwa hupata hitirafu ya kina saba ambacho uhusika katika kutengeneza chembe chembe nyekundu za damu,” alieleza Dkt Stella.

Athari za ugonjwa huu ni pamoja na mgonjwa kupungukiwa damu mara kwa mara, kuwa na maumivu makali yanayohitaji kulazwa, kuharibu maungo ya ndani ikiwemo kupata kiharusi, moyo kushindwa kufanya kazi vizuri, ini kufeli ambao hali hii huleta hali mbaya kwa mgonjwa na hupelekea kurudisha nyuma ukuaji wa mtoto.

“Naomba kuwasihi wazazi wenye Watoto wanaosumbuliwa na ugonjwa wa selimundu kufika Hospitali mapema ili kupata muongozo wa namna ya kusaidia mtoto ili apate matibabu kwa haraka,” alisisitiza Dkt. Stella.

Kwa upande wake Joseph John mzazi wa Elisha John ameeleza changamoto alizokuwa akipitia mtoto wake kabla ya kupandikizwa Uloto (Bone Marrow transplant).

“Mtoto wangu amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa selimundu kwa kipindi cha miaka kumi na moja tatizo kubwa alilokuwa akipata ni kupungukiwa damu kila baada ya wiki mbili, kuumwa tumbo, kupata joto na kukosa hewa,” alieleza Ndg. Joseph

Ndg. Joseph anaeleza kuwa kabla ya mtoto wao kupandikizwa uloto walipata changamoto na wasiwasi kwani ilikua ni mara ya kwanza Huduma hii kutolewa nchini.

“Naishukuru serikali kwani hatujachangia chochote kwenye kupata huduma hii na mtoto alikaa Hospitali kwa kipindi cha miezi mitatu na amepona kabisa na hatujapata changamoto yoyote ya kiafya tokea atoke Hospitali,” alieleza Ndg. Joseph.

Serikali ya awamu ya sita imefanya uwekezaji mkubwa hivyo wazazi wenye Watoto ambao wanasumbuliwa na ugonjwa wa selimundu wafike BMH kupatiwa matibabu na pale inapofaa kupandikiziwa uloto (Bone Marrow transplant).