Mwanzo / Huduma Zetu / KOFIH YA FURAHISHWA MIUNDOMBINU HUDUMA ZA DHARURA-BMH

KOFIH YA FURAHISHWA MIUNDOMBINU HUDUMA ZA DHARURA-BMH

Published on May 30, 2023

Article cover image

May 30,2023 Dodoma,

Profesa Kang Hyun Lee wa shirika la Korea Foundation for International Healthcare (KOFIH) linalojihusisha na kutoa misaada ya huduma za Afya na mahusiano la Korea Kusini amefurahishwa na miundombinu na mifumo ya kutolea huduma kwa wagonjwa wa dharura na mahututi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa hapa jiji Dodoma.

Akiwasilisha mada kuhusu uzoefu huduma za wagonjwa wa dharura na mahututi kwa madaktari na wauguzi wa Idara ya Magonjwa ya dharura wa BMH, Profesa Lee amesema kuwa kipindi cha vita (1950-53) huduma za dharura zilikuwa katika kiwango cha chini sana nchini mwao, majeruhi walipoteza maisha na magonjwa ya kuambukiza yalikatili watu wengi uhai.  

Hata hivyo, baada ya vita huduma za dharura ziliimarishwa nchi humo, ikiwemo kuwa na idadi kubwa ya magari ya wagojwa ili kuwafikia mapema na kuwapa huduma kabla hawajafika Hospitali, na wanapofika kupelekwa sehemu sahihi wanakopata matibabu sahihi kwa wakati sahihi.

“Hapa kuna dharura nyingi hasa za kina mama na wajawazito, miundombinu yenu imepangiliwa vizuri sana, mifumo yenu ya kutoa huduma iko vizuri, mnaweza kuokoa Maisha ya watanzania, kwa kuwa huduma za dharura zimeanzishwa miaka mitatu iliyopita, siku za usoni mifumo yenu inaweza kuokoa uhai wa watu wa nchi nyingine za Afrika” Alisema Profesa Lee.

Kwa upande wake Dkt. George Dilunga, Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Mkuu wa Idara ya Huduma za Dharura na wagonjwa Mahututi katika Hosptali ya Benjamin Mkapa amesema wasilisho la Profesa Lee limewapa mafunzo mengi ikiwemo kuboresha huduma za wagonjwa kabla hawajafika hospitali, yaani huduma za magari ya wagonjwa (ambulance services).

“Jambo lingine muhimu ni kuboresha huduma za wagonjwa wa dharura wanaokuwa Hospitali, itatuhitaji kuongeza bajeti kwa ajili ya kutoa mafunzo ya huduma za dharura kwa watoa huduma ili kuwaongezea ufanisi” Alisema Dkt. Dilunga.  

Itakumbukwa hivi karibuni Mhe. Ummy Mwalimu (Mb), Waziri wa Afya alidokeza kuwa serikali imenunua idadi kubwa ya magari ya wagonjwa ili kuimarisha huduma za dharura na wagonjwa mahututi hapa nchini.

Professor Lee amebobea katika huduma za magonjwa ya Dharura, pia ni Mkurugenzi wa taasisi ya tafiti za tiba zinazotumia teknolojia mpya katika Chuo Kikuu cha Yonsei, ameambatana na maprofesa wenzake 5 waliyobobea katika Huduma za Dharura, Uzazi, Mama na Mtoto (Obstetrics & Gynecology), Pamoja na Usingizi, Ganzi na Maumivu wote kutoka Shirika la KOFIH nchini Korea ya Kusini katika ziara ya siku mbili ya kufuatilia mwenendo wa madaktari wa waliyopata mafunzo kwa Ufakdhili wa shirika hilo.