BMH, UDOM NA TOKUSHUKAI KUJENGA KITUO CHA UMAHIRI CHA UPANDIKIZAJI FIGO
Published on April 06, 2025

Na Ludovick Kazoka, Dodom Machi 26 PICHA: Gladys Lukindo
Katika jitihada za kuifikia ndoto ya Serikali kuifanya Dodoma kuwa mji wa tiba utalii, Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) inapanga kujenga Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Figo kitakachogharamiwa na Shirika la Afya la Tokushukai la Japan.
Kituo cha kwanza maalumu nchini cha upandikizaji figo kitakuwa na vyumba vya kufanyia oparesheni na vyumba vya kulaza wagonjwa wa figo.
Kwa mujibu wa Afisa anayeshughulika na masuala ya Afrika wa Shirika la Tokushukai, Prof Mwanatambwe Milanga, utekelezaji wa mradi huo unaanza mwaka huu baada ya kusaini hati ya makubaliano na Serikali.
"Ujenzi unatarajiwa kukamilika 2028. Baada ya kukamilika kwa kituo hiki kitahamasisha madaktari vijana nchini," amesema Prof Milanga baada ya timu ya wataalamu kutoka Shirika la Tokushukai kukamilisha tathimini ya ujenzi huo BMH leo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof Abel Makubi, ameshukuru Shirika la Tokushukai kwa ushirikiano na BMH.
"Tupo tayari kutoa ushirikiano mkubwa wakati wa utekelezaji wa mradi huu wa ujenzi," amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali.