Mwanzo / Huduma Zetu / BMH YACHANUA MIAKA MIWILI YA Dkt. SAMIA SULUHU HASSAN

BMH YACHANUA MIAKA MIWILI YA Dkt. SAMIA SULUHU HASSAN

Published on February 24, 2023

Article cover image

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma Dkt. Alphonce Chandika ametoa tathimini ya mafanikio ya Hospitali hiyo ndani ya miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita.

Katika tathimini yake hiyo kwa waandishi wa Habari jijini Dodoma, Dkt. Chandika amesema kuwa hatua mbalimbali zimepigwa katika utoaji wa huduma za kibingwa bobezi ikiwemo huduma za Upandikizaji wa Figo, Matibabu ya Moyo, Mishipa ya Fahamu na Ubongo na vipandikizi kwenye Nyonga na Magoti.

“Ndani ya kipindi hicho tumewanufaisha wananchi 31 kwa kuwapandikiza Figo, wananchi 53 wamenufaika na huduma za vipandikizi vya Nyonga na Magoti na zaidi ya wananchi 900 wamenufaika na huduma za upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu” Alieleza Dkt. Chandika.

Aidha, ndani ya kipindi hicho cha miaka miwili ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Hospitali hiyo imepokea fedha za maendeleo zilizowezesha uboreshaji wa miundombinu na ununuzi wa vifaa tiba na vitendanishi ili kuboresha huduma za Afya.

Tulipokea zaidi ya bilioni mbili kutoka fungu lililotokana na fedha za IMF, UVICO-19, fedha hizo zimetusaidia kufanya maboresho ya Chumba cha Uangalizi Maalumu, kununua vifaa tiba vya Chumba hicho pamoja na vile vya huduma za dharula na majeruhi.

Dkt. Chandika amesema kuwa mbali na kuboresha miundombinu na ununuzi wa vifaa tiba, fedha hizo zimewezesha mafunzo kwa wataalamu wa huduma za dharula, uangalizi maalumu na radiolojia, Pamoja na kununua magari mawili ya wagonjwa.

Katika miaka hiyo miwili Dkt. Chandika amesema kuwa, serikali imenunua nyumba za watumishi wa Hospitali hiyo, Mtambo wa kuzalisha hewa tiba ya oksijeni na imenunua gari la kusafiri watumishi waendapo na kutoka kazini.

Akifafanua kuhusu Mipango ya siku zijazo, Mkurugenzi huyo amesema, Hospitali hiyo, inajenga kituo cha matibabu ya saratani, itaanzisha huduma za kupandikiza Uloto, kituo cha matibabu ya Moyo, Kituo cha Matibabu ya Ubongo na Mishipa ya Fahamu, kituo cha kupandikiza viungo, kituo cha mama na mtoto miongoni mwa miradi hiyo mradi wa ujenzi wa kituo cha Matibabu ya Saratani unaendelea.

Eneo lingine alilogusia ni kuhusu ushirikiano wa kimataifa ambapo amemshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha mahusiano ya kimataifa, kwa kuwa imetoa fursa kwa Hospitali yake kuanzisha ushirikiano na Taasisi za Afya na Hospitali mbalimbali kutoka ngambo yanayolenga kuanzisha na kuimarisha huduma za Ubingwa bobevu Hospitalini hapo.