Mwanzo / Huduma Zetu / BMH YAPELEKA HUDUMA ZA DHARURA KATESHI

BMH YAPELEKA HUDUMA ZA DHARURA KATESHI

Published on December 05, 2023

Article cover image

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imepeleka timu ya wataalamu katika mji wa Katesh kuongeza nguvu za huduma za Kiafya za dharura kwa manusura wa Mafuriko na Maporomoko ya aridhi yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.

Dkt. George Dilunga, Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura BMH ameongoza timu ya Madaktari na Wauguzi kuelekea Kateshi, Hanang Mkoani Manyara mapema leo.

“Tunakwenda kuhakikisha tunatoa msaada wa huduma za dharura kwa manusura, pamoja na sisi tumebeba vifaa vitakavyohitajika, zikiwemo dawa za aina mbalimbali zinazohitajika katika dharura ya namna hiyo” Amesema Dkt. Dilunga.

Disemba 4, Mheshimiwa Dkt. Godwin Molleli, Naibu Waziri wa Afya alitoa taarifa ya huduma za Afya huko Kateshi, pamoja na mambo mengine alitaja utayari wa Wizara kutoa huduma za Afya ambapo majeruhi 93 walikuwa wakipokea huduma katika hospitali na vituo mbalimbali vya Afya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Queen Sendiga, hadi kufikia asubuhi ya leo, watu 63 wamethibitika kupoteza Maisha kutokana na athari za mafuriko na maporomoko ya aridhi yaliyotokea mwishoni mwa wiki.