Mwanzo / Huduma Zetu / WANANCHI WAFAIDIKA NA HUDUMA BANDA LA BMH

WANANCHI WAFAIDIKA NA HUDUMA BANDA LA BMH

Published on April 06, 2025

Article cover image

Na Ludovick Kazoka, Dodoma Aprili 6, 2025

Wananchi mbalimbali wamefaidika na huduma ya bure ya vipimo na matibabu  katika banda la Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) katika viwanja vya ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma kwenye Wiki ya Afya.

BMH kwenye banda lake wanatoa huduma ya magonjwa ya dharura, mfumo wa mkojo, magonjwa ya damu, macho, vipimo vya ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu.

Bi Rhoda Alfayo, mkazi wa Ipagala, jijini Dodoma, ameshukuru kwa huduma na ushauri aliopata katika banda la BMH.

"Huduma na ushauri niliopata hapa bandani ni nzuri ina maana nisingekuja hata hivi vipimo na ushauri nisingevipata," amesema Bi Rhoda.

Bi Faith Kusaya, mkazi wa Iringa, anasema kuwa amepatiwa huduma ya bure  kuanzia vipimo mpaka matibabu.

"Serikali waendelee kutuletea matukio ya afya kama haya maana yanatusaidia kupata huduma za bure za vipimo," amesema Bi Faith.

Ndugu Adamu Mwakijo, mkazi  wa Chang'ombe, jijini Dodoma amesema amenufaika na vipimo vya kisukari na shinikizo la damu.

"Nimefaidika na vipimo vya kisukari na shinikizo la damu nimepata pia ushauri vyote hivi nimepata bure," amesema Ndg. Mwakijo.

Ndugu Fabian Chidawali, mkazi wa kijiji cha Mtitaa, wilaya ya Bahi, anasema amefanyiwa vipimo vya macho vya bure.

"Ina maana nisingekuja hapa nisingeweza kupata huduma hii, hivyo nawashukuru watoa huduma wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa huduma hii ya bure," amesema Ndg. Chidawali.