Mwanzo / Huduma Zetu / MAMIA WAJITOKEZA KUPATA HUDUMA ZA UBINGWA WA JUU BMH

MAMIA WAJITOKEZA KUPATA HUDUMA ZA UBINGWA WA JUU BMH

Published on April 07, 2025

Article cover image

Ludovick Kazoka, Dodoma  Aprili 7 PICHA: Jeremiah Mwakyoma 

Mamia ya wananchi wamejitokeza kupata huduma za afya za ubingwa wa juu katika banda la Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) katika Wiki ya Afya inayoendelea katika viwanja vya Jakaya Kikwete  jijiji Dodoma.

Tukio hili la Wiki ya Afya liliandaliwa na Wizara ya Afya limepongezwa kuwa ni tukio linalowapa wananchi fursa ya kupata huduma za afya za bure.

Bi Naomi Kimbindu, mkazi wa Kibaha, Pwani, anasema amefurahishwa na huduma alizopata Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH).

"Baada ya huduma hapa bandani nimeambiwa napaswa niende Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa vipimo zaidi, nimekuwa na tatizo la kupungukiwa damu mara kwa mara.Kesho ntakuja BMH kwa ajili ya vipimo zaidi," amesema Bi Naomi.

Bi Rehema Mwaluko, mkazi wa Nzuguni, jijini Dodoma anasema huduma ni nzuri, akisema tukio hili la Wiki ya Afya limempatia fursa ya kupata huduma za afya za bure.

"Nimefanya vipimo bure kabisa na nimepata ushauri wa kiafya," amesema Bi Rehema.

Bi Aneth Zabroni, mkazi wa Nkuhungu, jijini Dodoma, anaiomba Serikali kuandaa tukio kama hili kila mwaka, akisema linawapatia wananchi wa kima cha chini kupata huduma za afya bure.

"Mimi ni mnufaika wa hizi huduma, nimepata huduma za bure hapa kwenye banda la Hospitali ya Benjamin Mkapa," anasema Bi Aneth.