MKUU WA HUDUMA ZA DHARURA WIZARA YA AFYA: NENDENI MKABORESHE HUDUMA ZA DHARURA
Published on April 06, 2025

Na Gladys Lukindo, Picha: Carine Senguji- Dodoma, Machi 26, 2025
Washiriki wa mafunzo ya critical care wametakiwa wakaboreshe huduma za dharura wanaporejea kwenye vituo vyao vya kazi.
Akiongea wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mkuu wa Huduma za Matibabu ya Dharura kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Erasto Sylvanus, amesema kuwa watoa huduma za dharura ndiyo wako kwenye eneo la mstari wa mbele wa kuokoa maisha ya binadamu.
"Magonjwa 10 yanayoongoza katika kupoteza maisha, yanaangukia katika watoa huduma za dharura," amesema Mkuu wa Huduma za Dharura kutoka Wizara ya Afya, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi wakati wa kufunga mafunzo hayo.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kushirikiana na Kituo cha Huduma ya Matibabu ya Magonjwa ya Dharura (EMSA) yamewakutanisha watoa huduma 80 kutoka Dodoma, Singida, Songwe, Iringa na Morogoro.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof Abel Makubi amewataka Washiriki kuhakikisha mafunzo hayo yanakuwa chachu ya mabadiliko katika kuboresha huduma ya Dharura.
"Nategemea mkitoka hapa mnaenda kuwa chanzo cha mabadiliko ya kuboresha huduma za dharura kwenye vituo vyenu," amesema Mkurugenzi Mtendaji wa BMH.
Aidha Mkurugenzi wa EMSA, Dkt Ramadhani Chunga, amesema mwaka huu EMSA wanapanga kuwapa mafunzo watoa huduma za afya 800.
"Mpaka kufikia leo, tayari tumeishatoa mafunzo kwa watoa huduma 136 tokea mwezi uliopita," amesema.
Akitoa neno la shukrani, Mwenyekiti wa EMSA, Dkt. Sylvester Faya, amesema kuwa zamani wafanyakazi wa afya waligoma sababu ya kukosa vifaa, lakini sasa Hospitali za Serikali zina vifaa na teknolojia kama unavyoona BMH.
"Hii inaleta uhitaji wa kuboresha ubora wa huduma. Huduma ya Dharura inaweza kuwa ni kwa ajili huduma ya Dharula tu lakini hii ni mtambuka kwa watoa huduma wote," amesema Mwenyekiti wa EMSA.