Mwanzo / Huduma Zetu / ITF YAISHIKA MKONO BMH

ITF YAISHIKA MKONO BMH

Published on September 19, 2022

Article cover image

ITF YAISHIKA MKONO BMH

 

Dodoma, Septemba 19, 2022

 

Na, Ramond Mtani.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt. Alphonce Chandika amepokea msaada wa kitanda maalumu kuboresha huduma za kujifungua kwa mama mjamzito mwenye ulemevu anapofika kupata huduma ya kujifungua katika Hospitali hiyo.

 

Dkt. Chandika amesema kitanda hicho chenye thamani ya shilingi milioni 1.3 kilichotolewa na taasisi ya Ikupa Trust Fund (ITF) kinaongeza miundombinu ya kujifungulia kwa mama mjamzito hospitalini hapo na kwamba kitaiwezesha Benjamin Mkapa  kuendelea kumhudumia mteja mwenye ulemavu kwa staha na usiri zaidi.

 

Kitanda hiki kitatusaidia sana kutoa huduma za kujifungua kwa mama mjamzito mwenye ulemavu kwa kuwa hapatakuwa na msongamano, kitatusaidia kuboresha chumba chetu maalumu cha kutolea huduma ya kujifungua mjamzito mwenye ulemavu”  amesema Dkt. Chandika.

 

Aidha, Dkt. Chandika ameishukuru taasisi ya ITF kwa kuichagua hospitali ya Benjamin Mkapa kuwa ya kwanza kupokea msaada wa kitanda cha aina hiyo, akiahidi kuendela kuboresha miundombinu ya chumba maalumu cha kujifungua wajawazito wenye ulemavu, kwa kuongeza miundombinu, ili hospitali yake iwe mfano bora kwa kutoa huduma zenye staha na heshima kwa mjamzito mwenye ulemavu.

 

Awali, akikabidhi msaada huo Mwenyekiti wa Ikupa Trust Foundation, Mh. Amon Mpanju ambaye pia ni Naibu katibu Mkuu  wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, amesema kuwa msaada wa kitanda hicho ni kuunga mkono maelekezo ya Mh. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, linalozitaka hospitali kutenga eneo maalumu la kutoa huduma ya kujifungua mama mjamzito.

 

“Tunaishukuru Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kutekeleza agizo hilo la Mheshimiwa Rais kwa kuwa tayari wanacho chumba maalumu cha kujifungua mjamzito mwenye ulemavu”  amesema Mh. Amon Mpanju.

 

Kwa upande wake muasisi wa taasisi ya ITF Mh. Stella Ikupa, ambaye pia ni Mbunge viti maalumu anaewakilisha walemavu, amesema kuwa walemavu wanayo mahitaji mengi ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa miundombinu rafiki wanapokuwa wakipatiwa huduma za Afya hasa za kujifungua.  

 

“Unajua jamii bado inamshangaa mlemavu akipata ujauzito, inasahau kuwa agizo la Mungu la kuzaa na kuijaza dunia ni hitaji la kila mmoja, ndiyo maana kuwepo chumba maalumu chenye miundombinu rafiki katika hospitali hii na nyinginezo, kutamfanya mjamzito mwenye ulemavu ajifungue kwa furaha bila kuhisi unyanyapaa” Amesema Mh. Ikupa.

 

Taasisi ya ITF inalenga kugawa vitanda vya kumsaidia mama mjamzito mwenye ulemavu kujifungua kwa Hospitali mbalimbali za rufaa nchini, hospitali ya Benjamin Mkapa imekuwa ya kwanza kupokea msaada huo.