Mwanzo / Huduma Zetu / ZAIDI YA WATOTO 700 WAPATIWA HUDUMA ZA UCHUNGUZI KWENYE KAMBI YA KUMUENZI DKT. GEORGE DILUNGA

ZAIDI YA WATOTO 700 WAPATIWA HUDUMA ZA UCHUNGUZI KWENYE KAMBI YA KUMUENZI DKT. GEORGE DILUNGA

Published on March 12, 2025

Article cover image

Na Carine Senguji, Machi 10 2025, DODOMA.

Zaidi ya watoto 700 wamepatiwa huduma za uchunguzi katika kambi ya kumuenzi aliekua daktari katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) George Dilunga ambapo kambi hii imeendeshwa kwa ushirikiano wa BMH na ABBOTT FUND Tanzania.

Akizungumza dkt. Julieth Kabengula amesema kuwa mpaka sasa takribani watoto 750 wamepata huduma za uchunguzi wa awali na wengi wao wana tatizo la lishe.

"Kambi yetu hii tumeianza Jumatatu Machi 3 katika shule ya msingi Ihumwa na leo tunatamatisha katika kituo cha watoto yatima kikombo ambapo dkt. George Dilunga alikua anakuja pamoja na madaktari wengine wa BMH kutoa huduma na katika kambi hii tumebaini asilimia 30 ya watoto wana tatizo la lishe haswa pale shuleni na hii haitofautiani sana na takwimu zilizotolewa na tume ya twakwimu," amesema dkt. Julieth.

Dkt. Julieth amebainisha ugonjwa mwingine ambao waliona unasumbua watoto shuleni ni pamoja na matatizo ya mzio (allergy) ambapo wengi wana tatizo la pumu ya ngozi.

"Wanafunzi wengi wana matatizo ya ngozi yani pumu ya ngozi na wengine wana ukurutu ambao unatokea sana sehemu ambazo kuna upungufu wa maji," ameongeza dkt. Julieth.

Kwa upande wake dkt. Winnie Msangi, Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura BMH ameshukuru ABBOTT FUND Tanzania kwa kuwezesha kambi ya kumuenzi dkt. George kuwa ya mafanikio makubwa.

"Tunashukuru ABBOTT FUND Tanzania kwa kutuwezesha kufanikisha kambi hii na wamekua wakifanya kazi kwa ukaribu na dkt. George Dilunga kwa muda mrefu haswa kwenye eneo la magonjwa ya dharura," amesema dkt. Winnie.

Msemaji wa familia Bw. Godfrey Kessy ameshukuru BMH na ABBOTT FUND Tanzania kwa kuandaa kambi hii kwaajili ya dkt. George Dilunga. 

"Nawashukuru sana BMH na ABBOTT FUND Tanzania kwa kuja na wazo hili la kufanya kambi ya kumuenzi mpendwa wetu na hii inaonesha ni jinsi gani mlifanya nae kazi vizuri kwenye majukumu yenu," amesema Bw. Geofrey.