Mwanzo / Huduma Zetu / Umuhimu wa Lishe Bora Katika Afya ya Binadamu

Umuhimu wa Lishe Bora Katika Afya ya Binadamu

Published on August 12, 2022

Article cover image

Lishe bora ni suala muhimu katika maisha ya kila siku ya binadamu kwasababu inasaidia kujiepusha na magonjwa mbalimbali hatari kama matatizo ya moyo, kisukari, matatizo ya figo, kansa.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa lishe kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Bi. Yasinta Luambano, ulaji wa mlo kamili  kila siku ni msingi mzuri wa afya bora kwa kila binadamu.

“Lishe ni matokeo ya hatua mbalimbali kuanzia chakula kinapoliwa, kinaposagwa, kumenge’nywa na hatimaye kufyonzwa mwilini ili kujenga afya bora ya mwili. Hivyo basi lishe bora hupatikana kwa kuzingatia mlo kamili na kwa muda sahihi,” amesema Bi. Luambano.

Lishe bora inahusisha kula mlo kamili kutoka kwenye makundi matano ya chakula lakini imekua tofauti kwa baadhi ya familia nyingi za kitanzania kwani kumekuwa na tabia ya kula chakula cha aina moja ambapo inasabisha watu kuwa na  hali ya lishe duni ambayo ndo kisababishi  kikubwa  cha  magonjwa  mbalimbali hatari.

“Makundi hayo ya chakula ni; nafaka, mizizi na ndizi mbichi (carbohydrates), vyakula asili ya nyama na jamii ya mikunde (protein), mbogamboga (vegetables), matunda (fruits) na kundi la mwisho ni mafuta, sukari na asali. Makundi haya ya chakula ndiyo yanayo tengeza mlo kamili ambao ndo unaleta lishe bora,” alieleza Bi. Luambano

Kila kundi la chakula lina faida yake mwilini alifafanua Bi. Luambano ambapo, Nafaka, mizizi na ndizi mbichi za kupika; Vyakula hivi vina wanga kwa wingi ambao huupatia mwili nishati lishe. Aina hii ya vyakula ni muhimu katika kuupa mwili nguvu za kufanya kazi mbalimbali. Vyakula vya aina ya nafaka ni mahindi, mchele, ngano, mtama, ulezi na uwele. Vyakula vingine ni aina ya mizizi na viazi kama vile muhogo, viazi vitamu, viazi mviringo, viazi vikuu, magimbi, ndizi za kupika na mashelisheli. Vyakula hivi pia vina protini, vitamini, na madini ingawa ni kwa kiasi kidogo.

 

Vyakula vya asili ya wanyama na jamii ya mikunde; Vyakula vya jamii ya mikunde, mbegu za mafuta na vyenye asili ya wanyama vina protini kwa wingi na ni muhimu katika kuujenga mwili na kuwezesha ukuaji wa mwili hasa kwa watoto. Vyakula hivi pia huupatia mwili nishati, vitamini na madini kwa kiasi kidogo. Vyakula vya asili ya wanyama na jamii ya mikunde ni pamoja na: nyama aina zote kama ile ya ng’ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe, kuku, bata, samaki na dagaa; Wadudu ni kama senene na kumbikumbi; mayai, maziwa na aina zote za kunde kama maharage, soya, dengu, kunde, choroko, njegere, mbaazi na njugu mawe na mbegu za mafuta mfano karanga, korosho, kweme, ufuta.

Mboga mboga; Mboga mboga huupatia mwili virutubishi vya vitamini na madini kwa wingi. Vitamini na madini huhitajika kwa kiwango kidogo sana lakini ni muhimu sana kwa mwili kuweza kufanya kazi zake vizuri na kuimarisha kinga ya mwili. Upungufu wa vitamini na madini mwilini unaweza kusababisha kinga ya mwili kudhoofika na kupata maradhi ya mara kwa mara mwilini. Vitamini na madini vinavyopatikana katika mboga mboga ni pamoja na Vitamini A,C,D,E,K na kundi la B ambalo lina B1,B2,B3,B6,B9 (asidi ya foliki), B12 na madini kama chuma (iron), chokaa (calcium) na zinki (zinc). 4 Mboga mboga zinajumuisha mchicha, majani ya maboga, majani ya kunde, matembele, kisamvu, figiri, karoti, mnavu, biringanya, maboga matango na mbogamboga nyingine za asili zinazopatikana eneo husika kama vile mchunga, mwidu, mlenda na majani ya mlonge.

Matunda; Kama ilivyo kwa kundi la mbogamboga, matunda ni muhimu sana katika mwili, kwa vile vyakula hivi vina vitamini kama vile A, B, C na madini mbalimbali ambayo ni muhimu kulinda mwili dhidi ya magonjwa. Mfano wa matunda ni chungwa, papai, nanasi, parachichi, zabibu, embe, pera na matunda ya asili yanayopatikana mahali husika kama vile ubuyu, ukwaju, na mabungo.

Vyakula vya mafuta, sukari na asali; Vyakula hivi huupatia mwili nishati lishe, huleta joto mwilini, na vile vile huleta nguvu mwilini, kulinda na kulainisha ngozi. Mafuta pia husaidia uyeyushwaji na ufyonzwaji wa vitamini A, D, E na K. Vyakula hivi pamoja na kutoa nishati huongeza ladha ya chakula. Mafuta ni pamoja na yale yanayotokana na wanyama mfano samli, siagi na yale yanayotokana na mimea mfano karanga, alizeti, nazi, ufuta, mbegu za pamba, korosho na mawese, kweme na mbegu za maboga. Kundi hili linajumuisha pia miwa, sukari na asali.

Kila binadamu anashauriwa kula mlo kamili mara tatu kwa siku, mahitaji ya kilishe hutofautiana kulingana na umri, jinsia na majukumu ya kila siku ya mwanadamu, mfano, mahitaji ya kilishe ya nishati lishe na protini kwa watoto hutegemea umri, uzito na kiwango cha ukuaji pia mtu anaefanya kazi ngumu mlo wake huwa tofauti na mtu ambaye anafanya kazi nyepesi lakini wote wanatakiwa kula mlo kamili.

Kwa upande wa watoto wazazi wanashauriwa kuwa makini sana katika suala zima la lishe kwani watoto huhitaji kupata mlo kamili wenye  virutubisho vyote vya kutosha vitakavyowasaidia katika ukuaji wao na tofauti na hapo mtoto anaweza kuwa na hali duni kilishe ambayo husababisha maradhi mbalimbali kama kudumaa kwa akili na mwili, uzito pungufu, kwashakoo na utapiamlo.

Kwa kutambua umuhimu wa lishe bora Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ina kitengo maalamu kinachotoa matibabu ya lishe chenye majukumu yote yanayohusiana na afya ya lishe kwa wagonjwa kwa upande wa tathimini za lishe, matibabu yote yanayohusiana na lishe, ushauri wa kimatibabu kwa upande wa lishe na kufuatilia kwa ukamilifu mambo yote yanayohusiana na lishe.

Bi. Luambano ameeleza kuwa kitengo cha lishe kinashirikiana kwa ukaribu na idara zingine za matibabu kwani kupitia idara hizo wagonjwa hutambulika na kisha kupewa rufaa ya ndani ili kupatiwa ushauri na matibabu ya lishe.

“Mgonjwa anapoletwa kwetu huwa tunamfanyia tathmini ya lishe kwa kuangalia mambo mbalimbali  kama , uwiano wa urefu na uzito (anthropometric), tathmini ya biokemikali (biochemical) ambayo hufanyika maabara pamoja na kupata tathimini ya lishe ya mgonjwa  (dietary assessment) na historia ya ulaji kwa mgonjwa (patient intake history). Na tukipata vipimo kamili ndipo tunampatia mgonjwa matibabu ya lishe na  ushauri  wa vyakula anavyotakiwa kutumia kulingana na changamoto ya afya  aliyonayo,” alieleza Bi. Luambano.

Takwimu mbalimbali zinaonesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha wananchi wake wanapata lishe bora na kupunguza vifo vya watoto vinavyotokana na lishe duni kwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa lishe bora na madhara yatokanayo na lishe duni.

Wataalamu wa lishe wanashauri mtu kupata kifungua kinywa kuanzia saa 1 asubuhi mpaka saa 2 asubuhi, chakula cha mchana kuanzia saa 6 mchana hadi saa 7 mchana na chakula cha jioni kuanzia saa 12 hadi saa 2 usiku.