Mwanzo / Huduma Zetu / TUNATIBU APONYAE NI MUNGU

TUNATIBU APONYAE NI MUNGU

Published on July 24, 2023

Article cover image

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kati Benjamin Mkapa (BMH) amewaomba viongozi wa dini kuendelea kuwaombea wagonjwa na watoa huduma za Afya nchini akisema kwa sababu madaktari wanaweza kutibu lakini mwenye uwezo wa kuponya ni Mungu pekee.

Dkt. Chandika ameyasema hayo leo alipotembelewa na ujumbe wa Jumuiya ya Maridhiano ya Mkoa wa Dodoma uliyofika Hospitalini hapo kutoa pongezi maalumu za kutambua mchango wa Hospitali hiyo katika utoaji wa huduma wenye kujali utu na kumfariji mgonjwa.

“Moyo wangu umejaa furaha sana kuwasikia mkitambua mchango wetu na wa serikali kufanya uwekezaji katika sekta ya Afya, ninaomba muendelee kutuombea wafanyakazi wa sekta ya Afya na wagonjwa kwani sisi tunachofanya ni kutibu tu, Mungu ndiye anaponya” Alisema Dkt. Chandika. 

Askofu Dkt. Evance L. Chande, ambaye ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Karmeli Assemblies of God na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Mkoa wa Dodoma alitumia rejea ya Biblia kutoka kitabu cha Luka 17:12-19 kuishukuru serikali ya awamu ya sita na Hospitali akisema yeye alihudumiwa vizuri, kwa kupewa maneno yenye faraja kutoka kwa watumishi.

“Nilipaswa niende India, kama serikali isingewekeza hapa huenda nisingekuwepo leo maana ugonjwa ulikuja ghafla, ingekuwa vigumu kukusanya fedha na kuwahi matibabu hayo nje ya nchi” Askofu Dkt. Chande.

Kwa upande wake Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Dodoma Shekhe Hussein Ramadhani Kazungu, ametoa ushuhuda wa namna alivyopokea matibabu baada ya kupata ajali, akisifia kauli nzuri na kutoa wito kwa wanadodoma kujivunia uwekezaji wa Serikali katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.

“Tunaona kwenye mtandao, tunashuhudia tukifika, wewe ni Mkurugenzi unayejitambua, hukai ofisini na unao watumishi wenye kauli nzuri wanatujenga kiimani” Sheikhe, Kazungu.

Ujumbe wa viongozi hao, uliambatana na Mheshimiwa Dkt. Alice Kaijage, Mwakilishi wa Wafanyakazi Bungeni ambaye alifurahishwa na taarifa Chanya kutoka kwa viongozi wa dini kwenda kwa wafanyakazi. 

“Ninawashukuru kwa jinsi mnavyoishi viapo vyenu, BMH mmenifariji sana, mmemvisha Ua Mheshimiwa Rais, mmeithaminisha serikali na Chama cha Mapinduzi” Alisema Mhe. Dkt. Kaijage. 

Benjamin Mkapa ni Hospitali inayotoa huduma za Uchunguzi na Matibabu ya kibingwa na Ubingwa bobezi hasa zile zilizokuwa adimu nchini.