Mwanzo / Huduma Zetu / TUTAKUWA MABALOZI WAZURI WA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA

TUTAKUWA MABALOZI WAZURI WA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA

Published on June 25, 2024

Article cover image

Na Gladys Lukindo , Dodoma, 24 June, 2024

Hayo yamebainishwa  na  Bi. Jackline Mangesho, Mkurugenzi wa Asasi ya Mystreet First (MSF) walipofanya ziara na Wanafunzi kutoka shule za Msingi na Sekondari zilizopo katika Kisiwa cha Mafia wametembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ili kujionea huduma za afya za kibingwa na ubingwa bobezi.

"Tumewaleta wanafunzi 25 hapa ili kujifunza huduma zinazotolewa hapa hospitali na tunawafundisha kuweza kupambania ndoto zao na pia tutatoa uelewa kwa watu wenye ndugu wanaoumwa Selimundu kuwa matibabu haya yanayotolewa Hospitali ya Benjamin Mkapa," amesema Bi. Jackline Mkurugenzi wa Asasi ya Mystreet First (MSF). 

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dkt Kessy Shija, amesema Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof  Abel Makubi, anatambua ujio wa wanafunzi hao na kwamba ziara hiyo itawasaidia kujifunza huduma za kibingwa na ubingwa bobezi zinazotolewa Hospitalini hapo.

"Nawashukuru kwa kuchagua kutembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa ambayo ni Hospitali ya pekee katika Afrika Mashariki na Kati inayopandikiza Uloto , (Tiba ya pekee ya Selimundu) tunafanya upasuaji wa moyo na kupandikiza figo,” Dkt. Shija amemnukuu Prof Abel Makubi, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali. 

Dkt. Shija amewataka wanafunzi hao kuwa mabalozi wazuri wa BMH na kueleza huduma zinazotolewa na BMH. 

Mwanafunzi kutoka Shule ya Sekondari ya Kitomondo, Said Yusuph ameishukuru  BMH kwa elimu waliyoipata na kuahidi kuwa watakuwa mabalozi wazuri wakirudi Mafia.

Wanafunzi hao wametembelea Kitengo cha Uchujaji Damu (haemodialysis) na kujifunza namna mashine za uchujaji damu zinavyofanya kazi na pamoja na Idara ya radiolojia na kujifunza kuhusu mashine ya CT-scan na mashine ya kupima kansa kwenye titi (Mamograph).