Mwanzo / Huduma Zetu / WALIOTIBIWA MACHO WAPEWA ELIMU YA KUYATUNZA

WALIOTIBIWA MACHO WAPEWA ELIMU YA KUYATUNZA

Published on June 05, 2023

Article cover image

Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma (BMH) wametoa elimu ya jinsi ya kutunza macho kwa wagonjwa walionufaika na huduma ya upasuaji kutoka kwa madaktari hao katika Hospitali ya wilaya ya Newala, Mtwara.

Akizungumza na wagonjwa hao Dkt. Amon Mwakakonyole Daktari Bingwa wa magonjwa ya macho kutoka BMH amewashuri wanufaika hao kuachana na vitu vitakavyopelekea kuathiri macho yao ambayo yamefanyiwa upasuaji. 

“Ili kutunza macho yenu na kuona tija ya upasuaji huu mnatakiwa kuachana na vitu vitakavyopelekea kuathiri macho yenu vitu hivi ni kama kutafuna vitu au vyakula vigumu, kuinama na kufanya kazi ngumu,” alieleza Dkt. Mwakakonyole.

Aidha, Dkt. Mwakakonyole amewatahadharisha wanufaika wa huduma ya Upasuaji kuwa makini endapo wataona dalili za viashiria vya hatari kwenye jicho lililofanyiwa upasuaji.

“ukipata maumivu makali ya kichwa, kuona jicho lina kama michanga na kutokuona mwanga baada ya upasuaji basi hizo ni dalili mbaya na unatakiwa kuwahi Hospitali kwaajili ya matibabu,” alisisitiza Dkt. Mwakakonyole.

Vile vile, Dkt. Mwakakonyole amewashauri wagonjwa ambao bado hawajawa na uoni mzuri wasife moyo kwani tatizo itachukua angalau miezi mitatu ili kurudisha uoni wao.

Kwa upande  wao baadhi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wameshukuru uwepo wa madaktari kutoka BMH na kuwashukuru kwa kuwarudishia uoni wao.

“Kabla ya upasuaji nilikua naona ukungu tu haswa nyakati za mchana ila baada ya kufanyiwa upasuaji na madaktari bingwa wa Macho kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa sasa hivi naona vizuri ile hali ya ukungu imetoweka kabisa, natoa wito kwa watu ambao bado hawajafika kupima macho waje kupata Huduma hii kwa gharama nafuu na ninaomba madaktari hawa waje mara kwa mara kutupatia Huduma,” alieleza Shabani Mnefi mkazi wa Newala, Mtawara.

kambi bado inaendelea na inatarajiwa kumaliza Juni 2, 2023.