Mwanzo / Huduma Zetu / WANAWAKE WASHAURIWA KUFANYA VIPIMO KABLA YA KUBEBA UJAUZITO

WANAWAKE WASHAURIWA KUFANYA VIPIMO KABLA YA KUBEBA UJAUZITO

Published on June 26, 2024

Article cover image

Na. Carine Abraham Senguji, Juni 26, 2024.

Watumishi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) wamepata mafunzo ya dalili zinazoashiaria mgonjwa kupata kifafa cha Mimba (preeclampsia). 

Mafunzo hayo yametolewa katika programu maalumu inayofanyika kila Jumatano, ikishirikisha watumishi kutoka idara zote za BMH inayojulikana kama Continues Medical Education (CME).

Dkt. Christopher Mzimya,  mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, UDOM, ambae anasomea magonjwa ya wanawake ameelezea kiundani dalili za ugonjwa huo.

"Ugonjwa huu una dalili za awali ambazo ni pamoja na mgonjwa ambae hajawahi kuwa na shinikizo la damu huko nyuma kupata shinikizo la damu kuanzia wiki ya 20 ya ujauzito na kukutwa na protini kwenye mkojo," amesema Dkt. Mziya.

Dkt. Mziya ameendelea kwa kusema kuwa dalili mbaya zaidi za ugonjwa huu ni shinikizo la damu kua juu kuanzia na kupungua kupata mkojo na hii inaashiria figo imeathirika.

"Mgonjwa anapokua na shinikizo la juu la damu kuanzia 160 kwenda juu na mkojo kupungua hadi 30mls kwa saa mgonjwa huyu anasemekana kuwa na hali mbaya pre-eclampsia na anaweza kupata kifafa cha mimba," amesema.

Dkt. Mziya ameendelea kwa kusema kuwa mwanamke anaweza kupata ugonjwa huu endapo atakuwa na mahusiano na wanaume tofauti tofauti na kuwa na umri mkubwa.

"Endapo mwanamke atakua na mahusiano na wanaume tofauti, kuwa na umri zaidi ya miaka 35 na kuwa na uzito mkubwa anahati kubwa ya kupata preeclampsia," amesema Dkt. Christopher 

Hata hivyo, Dkt. Mziya, ameainisha njia kadhaa za kujikinga na ugonjwa wa preeclampsia.

"Kabla ya kubeba ujauzito mwanamke anatakiwa kufanya vipimo ili kujua kama ana shinikizo la damu, kisukari na wenye umri mkubwa wanashauriwa kutumia doze ndogo ya aspirini na kutumia dozi ya calcium ili kuepuka kupata preeclampsia kipindi cha ujauzito," ameeleza Dkt. Christopher. 

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Bi. Prisca Lwangili amependekeza elimu hii kufikia watu wengi katika jamii kupitia vyombo vya habari na maandiko ili kuondokana na dhana potofu ambazo zipo katika jamii zetu kama uchawi.

"Napendekeza elimu hii ifikie watu wengi katika jamii haswa vijana ambao wapo katika kipindi cha kupata watoto na hii itasaidia kuokoa maisha ya watu wengi katika jamii zetu," amesema Bi. Prisca.